Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Odinga, waahidi kuwaunganisha Wakenya


Bw Kenyatta na Bw Odinga wameahidi kuwaunganisha Wakenya
Image captionBw Kenyatta na Bw Odinga wameahidi kuwaunganisha Wakenya
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo Raila Odinga katika afisi yake Jumba la Harambee, Nairobi.
Wawili hao wamekubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa rasmi karibuni
Balozi Martin Kimani ataongoza kuundwa kwa mpango huo upande wa Rais Kenyatta naye mshauri wa Bw Odinga Paul Mwangi atawakilisha Bw Odinga, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Bw Kenyatta na Bw Odinga baada ya mkutano huo.
Mkutano huo umefanyika muda mfupi kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.
Marekani imekuwa ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo baada ya uchaguzi uliojaa utata mwaka jana.
Bw Odinga alitangulia kuhutubia taifa moja kwa moja na baadaye Bw Kenyatta akatoa hotuba yake.
Bw Kenyatta amesema wamekubaliana na Bw Odinga kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.
Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."
"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze."
"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna araia anayehisi ametengwa."
"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu."
"Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya."
Bw Odinga amesema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.
"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Bw Odinga.
"Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa lililofeli."
Bw Tillerson atawasili nchini Kenya baadaye leo

Comments

Popular posts from this blog

Mvua yatatiza mpambano kati ya Simba SC na El Masri

Marubani Wawili Wapoteza Maisha kwa Ajali ya Ndege Zanzibar

Huduma za serikali ya Marekani zakwama kwa mara nyengine