
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akijibu swali la Mbunge wa
Kyerwa Innocent Sebba Bilakwate leo Bugeni Mjini Dodoma lililohoji ni
lini Serikali itawapatia Wananchi wa Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio
TBC ili kujua yanayoendelea katika nchi yao kama ilivyokuwa hapo awali
kabla ya kubadilisha teknolojia ya habari badala ya sasa kusikiliza
Redio Rwanda na Uganda.
Picha na Frank Mvungi, MAELEZO,
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
Serikali imeanza kutekeleza
Mpango wa kujenga mitambo ya FM nchini kuimarisha usikivu maeneo
mbalimbali ili wananchi waweze kupata matangazo kutoka redio yao ya
Taifa (TBC).
Kauli hiyo imetolewa leo
Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Anastazia Wambura alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa
Innocent Sebba Bilakwate kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, lililohoji ni lini Serikali
itawapatia Wananchi wa Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio TBC ili kujua
yanayoendelea katika nchi yao kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya
kubadilisha teknolojia ya habari badala ya sasa kusikiliza Redio Rwanda
na Uganda.
Mpango huo unatekelezwa na
Serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambao umeanza
kutekelezwa katika wilaya za Kibondo, Nyasa, Longido, Tarime pamoja na
Rombo na utaendelea katika wilaya nyingine ikiwemo Kyerwa kadiri bajeti
inavyoendelea kuimarika.
“Kwa sasa kama ilivyobainishwa
katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya mwaka 2017/2018, Serikali
inaendelea kubadilisha mfumo wa urushaji matangazo kupitia satelaiti
uweze kuwa wa kisasa ili kuboresha usikivu wa radio ya Taifa TBC hatua
itakayosaidia wananchi kuendelea kupata habari kupitia viongozi wao”
amesema Naibu Waziri Wambura.
Naibu Waziri Wambura
amebainisha kuwa zipo wilaya 84 nchini ambazo usikivu wa TBC umeshuka na
kusababisha baadhi ya maeneo kukosa matangazo ya redio kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa baadhi ya miundombinu ya radio,
uwepo wa milima na uharibifu wa vifaa kutokana na radi wakati wa mvua.
Aidha, Naibu Waziri Wambura
amewataka Wabunge na wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa
kutoa taarifa endapo kutatokea uharibifu wa vifaa vya kusaidia
upatikanaji na usikivu wa matangazo ya radio ya taifa TBC katika maeneo
yao ili yaweze kufanyiwa marekebisho mapema na wananchi waendelee kupata
habari mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa.
Wilaya ya Kyerwa iko katika Mkoa
wa Kagera ambapo matangazo ya Redio yanapatikana kupitia mtambo wa TBC
ulioko katika Manispaa ya Bukoba ambao unasafirisha mawimbi ya Redio
katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Comments
Post a Comment