MGAHAWA MWEKUNDU WA MAN UNITED UNAVYOINGIZA MAMILIONI KWA SIKU
Na Saleh Ally, Manchester
NIMEFANYA
ziara mara kadhaa katika timu mbalimbali zikiwemo zile kubwa kabisa
duniani kutoka katika ligi maarufu Ulaya na duniani kote.
Kama
unakumbuka nimefanya hivyo Ujerumani nikipata nafasi ya kufika katika
Klabu ya Frankfurt na Borussia Dortmund na baadaye Hispania
nilipotembelea na kujifunza kupitia Atletico Madrid, FC Barcelona na
Real Madrid.
Ninapojifunza
inakuwa ni kwa ajili ya wasomaji wa gazeti hili bora la michezo na
burudani la Championi, kwa kuwa safari ndefu ya saa zaidi ya 10, mara
zote unapotoka Afrika hadi Ulaya, si jambo dogo.
Safari
hii nimesafiri kwa takriban saa 24, nikiwa na safari ndefu kutoka Dar
es Salaam, Nairobi, Abu Dhabi na baadaye jijini Manchester, England
ambako safari nyingine inayonijumuisha mimi na wewe inaanzia hapa.
Nimeanzia
katika Klabu ya Manchester United ambako nimepata mwaliko kutoka kwa
Klabu ya FC Barcelona ambao wamekuja hapa kucheza mechi ya kirafiki
dhidi ya Manchester United, ni mechi ya wakongwe.
Si
rahisi nifike hapa na kutojifunza mambo mengi na siku moja kabla ya
mechi hiyo iliyochezwa jana, nilifika hadi kwenye Uwanja wa Old Trafford
ulio katika eneo la Trafford jijini hapa kujifunza mengi.
Moja
ya mambo ambayo yamenifurahisha na huenda mashabiki wa soka wa nyumbani
wanaweza kukubaliana nami kuwa ni jambo la kawaida lakini lina ubunifu
wa juu kabisa, linaweza kufanyika nyumbani na kuzisaidia klabu zetu
mbalimbali kuingiza fedha, ni hili la mgahawa wa Manchester United.
Ndani
ya Uwanja wa Old Trafford kuna mgahawa uitwao Red Cafe, kwa Kiswahili
ni Mgahawa Mwekundu. Uko katika ghorofa ya tatu ya uwanja huo na zaidi
unatumiwa na mashabiki ambao hufika kuutembelea uwanja huo katika sehemu
yake ya makumbusho.
Mgahawa
huo upo upande wa jukwaa la Alex Ferguson ambalo ndilo jukwaa kubwa
zaidi na linaloingiza watu wengi zaidi katika uwanja huo mkubwa zaidi
nchini England kwa viwanja vinavyomilikiwa na klabu. Old Trafford inaingiza watazamaji 75,643.
Lakini
unatumiwa na mashabiki baadhi wanaokwenda katika mechi zinazochezwa
kwenye uwanja huo na nimesema wachache kwa kuwa ni wale ambao tiketi zao
huwa ni VIP na tayari wamelipia kupata huduma ya vinywaji na vitafunwa.
Baadhi
ya tiketi tayari zinakuwa zimejumlishwa na huduma hiyo na hapo ndiyo
utaona uhakika unapoanzia kwa Mgahawa Mwekundu kwa kuwa una uhakika wa
kuuza katika kila mechi hata kama baadhi ya mashabiki watakuwa
hawajafika, basi fedha huingia ndani ya mgahawa kulingana na idadi ya
tiketi zilizokatwa na si wateja wangapi walikwenda kuangalia mechi siku
hiyo.
Katika kila mchezo, mgahawa huo unaweza kuingiza hadi pauni 25,000
(zaidi
ya Sh milioni 72), jambo ambalo si rahisi hata kwa hoteli kubwa za
Tanzania kuingiza robo ya fedha hizo mara moja unapozungumzia huduma ya
chakula na vinywaji pekee.
Mmoja
wa wahudumu, amesema ingawa si rahisi kujua mahesabu ya kila siku, bila
ya kuwa na mechi huingiza hadi pauni 18,000 (zaidi ya Sh milioni 52),
mambo yanapokuwa si mazuri sana na kama kipindi cha baridi kali,
huingiza pauni 5,000 hadi 8,000 ambacho bado ni kiwango kikubwa cha
mauzo kwa migahawa mingine.
Kinachowavutia
watu wengi kuingia katika mgahawa huo, kwanza ni kwa kuwa uko katika
sehemu maarufu, yaani Uwanja wa Old Trafford ambao una jina kubwa
duniani kote.
Ukiwa
katika Jiji la Manchester, Old Trafford ni kivutio cha utalii na wengi
hasa wageni wanaofika kutoka hapa barani Ulaya, Asia, Afrika na
kwingineko duniani, wangependa kufika angalau hata kuuona ‘Live” kwa
kuwa wamechoka kuuona mubashara kwenye runinga.
Katika
mgahawa huo mwekundu, asilimia 80 ya viti vyake vimebandikwa majina ya
wachezaji wa timu hiyo yenye mafanikio zaidi ya ushindi wa vikombe
katika Ligi Kuu England.
Viti vina majina ya wachezaji na namba zao. Unaanza na wachezaji walio katika kikosi cha sasa chini ya kocha Jose Mourinho.
Lakini
kuna viti vyenye majina ya wachezaji wengi nyota wa zamani kama Rio
Ferdinand, Peter Schmeichel, Eric Cantona, Ryan Giggs, David Beckham,
Wayne Rooney na wengine kibao.
Mvuto
zaidi, unaonekana kwa wengi ni wachezaji walio Man United kwa sasa kama
Zlatan Ibrahimovic, Anthony Martial, Marcus Rashford, Romelu Lukaku,
Paul Pogba, David de Gea na wengine.
Mashabiki
hupenda kuchagua kukaa katika kiti cha mchezaji anayemvutia zaidi. Kama
kimepata mtu basi anaweza kuangalia kingine kwa kuwa jina moja linaweza
kuwa na viti viwili, vitatu au vinne.
Lakini
bado mteja anaweza kuwa na nafasi ya kuchagua mchezaji anayefuatia kwa
kumpenda na zaidi na zaidi. Hiyo inakuwa ni katika kujifurahisha.
Kitaalamu inaonyesha mteja hujiona yuko sehemu sahihi na aliyoitaka na wakati
mwingine hujiona kama anajumuika na watu anaowapenda kwa kuwa majina
yao yamemzunguka, hivyo kumfanya ni mwenye amani na kufurahia zaidi
sehemu aliyopo.
Kwa
Simba na Yanga zenye mashabiki wengi, jambo hili linaweza kuwa la
kujifunza. Kuiga kitu bora na ikiwezekana na kukiboresha zaidi si kitu
kibaya. Maana wana wateja lakini hawawaingizii lolote, nimekuwa
nikilizungumzia hili mara kwa mara.
Pia hawawatumii wachezaji wao vizuri kuingiza wanachotaka kibiashara.
Huenda
hawana watu sahihi wa masoko au hawajajifunza zaidi katika masoko ya
soka na wanaweza wakawa wanawapa ushauri katika biashara lakini
wasilenge mlango sahihi unaoweza kuwa na faida kupitia soka kama
wanavyofanya Manchester United.
Wanaingiza
mamilioni ya fedha, hii ni sehemu ya utajiri wao unaowafanya wamsajili
wanayemtaka lakini kulipa inavyotakiwa na kuwafanya wachezaji wao kuwa
na furaha zaidi, waifanye kazi yao sahihi na kuendelea kuifanya Man
United kuwa maarufu na kubwa zaidi.
Comments
Post a Comment