YANGA MWENDO MDUNDO MSIMU WA 2017-18

Samuel Samuel
Mabingwa wa soka Tanzania bara leo
wanaingia kambini rasmi kisiwani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya
fainali ya kombe la Ngao ya jamii na mwanzo wa ligi kuu Tanzania bara
inayoanza mwishoni mwa mwezi huu wa nane tarehe 27.
Tarehe 23 August 2017, Yanga
watakuwa uwanja wa taifa na washindi wa kombe la FA ( ASFC ) kwenye
mtanange wa kugombania Ngao ya jamii. Hii ni mechi ya ufunguzi wa ligi
kuu nchini inayowakutanisha watani wa jadi baada ya misimu kama minne
hivi kukutana katika Ngao ya jamii.
Yanga waliokuwa kambini Morogoro
kabla ya kucheza mechi tatu za kirafiki wakipoteza moja dhidi ya Ruvu
Shooting na kushinda mechi mbili dhidi ya Singida United 3-2 na Mlandege
ya Zanzibar 2-0; leo wanaingia kisiwani Pemba kujifua kwa mara ya
mwisho kabla ya kuanza ligi.
George Lwandamina kocha mkuu wa
Yanga inaonesha msimu huu atakuwa na kipaumbele cha kutumia damu changa
kikosini mwake katika kuimudu mikikimikiki ya ligi kuu Tanzania bara.
Licha ya ujio wa kiungo wa timu
hiyo Pappy Tshishimbi aliyesajiliwa kutoka Mbabane Swallows kusuasua
mpaka sasa ; tayari muunganiko wa kinda Maka Edward aliyetoka timu B na
Rafael Daudi aliyesajiliwa toka Mbeya City unaonesha kuleta uhai katika
kikosi cha wanajangwani hao.
Uwezo kisoka kwa maana ya kutimiza
majukumu yake kama kiungo mkabaji , nguvu, kujiamini na uelewano mzuri
na wenzake unamfanya Maka Edward kusimama kama silaha muhimu kwa
Lwandamina msimu wa 2017-18.
Bado Saidi Makapu anaonekana
kukosa muendelezo mzuri mbele ya Maka na asipokuwa makini kinda huyo
anaweza kumpoteza katika nafasi hiyo ambayo mara nyingi mkongwe Thabani
Scara Kamusoko huiweka chini ya himaya yake.
Ramadhani Kabwili kijana wa miaka
18 anaonesha kuiva vyema katikati ya miamba Youthe Rostand na Beno
Kakolanya. Huyu anatarajiwa kusimama kama nguzo muhimu katika kikosi cha
mzambia huyo. Kipa namba moja wa kikosi hicho Beno Kakolanya anauguza
majeraha ambayo aliyapata timu ya taifa hivyo ni yeye na Rostand ndio
wenye dhamana ya kulilinda lango la timu hiyo.
Msimu wa 2013-14 Simba SC
waliibuka na kinda Manyika Jr akiwa na umri sawa na Ramadhani Kabwili
kwa sasa lakini aliweza kusimama imara kwenye kikosi cha timu hiyo .
Octoba 18 2014 aliweza kulilinda vyema lango la Simba mbele ya Yanga
iliyokuwa moto wa kuotea mbali kwa sare ya 0-0 hivyo sioni shida kwa
Yanga kumuamini Kabwili dhidi ya mnyama huyo tarehe 23 pia kuanza nae
kwenye ligi. Ni dhahiri kambi ya Pemba benchi la ufundi litatumia muda
wa kutosha kumuandaa kipa huyu.
Bado Lwandamina na jopo lake wana
nafasi nzuri kutetea taji lao kwa aina ya wachezaji walionao endapo
umakini na maandalizi ya kutosha yatafanyika kuanzia Pemba kuja bara.
Ibrahimu Ajibu, Donald Ngoma ,
Amisi Tambwe , Emanuel Martini na Obrey Chirwa si safu ya kubeza kwenye
forwad line ni kiasi cha kutafuta muunganiko wao mzuri kwa mbinu na
mifumo watakayo tumia . Safu hii inategemea uimara na uwezo kimbinu ya
viungo nyuma yao na kwenye flanks pia wing backs.
Emanuel Martin anaetumika sana
kama winga wa kulia katika mechi hizi tatu za kirafiki na mazoezini kule
Morogoro anaonesha kujipanga vyema msimu huu. Lwandamina anaweza
kumfanya mpishi katika pacha ya Ngoma na Tambwe kulia akisimama Yahya
Akilimali au Yusufu Muhilu. Ana uwezo wa kufunga kutokea pembeni pia ans
uwezo wa kuwacheza washambuliaji wa kati kutokea pembeni au kuingia
kati nakufanya technical screening kwa washambuliaji wa kati kufunga.
Piusi Baswita ni ingizo jipya
katika kikosi cha wanajangwani hao . Ni kiungo ambaye ana uwezo mzuri
kwa maana ya kipaji halisi lakini benchi la ufundi la Yanga SC
linahitajika kuitumia kambi ya Pemba kumjenga kucheza mpira kwa manufaa
ya timu. Kucheza mpira wa kuamua matokeo chanya kwa timu pia kulinda
mifumo yote miwili ya timu ; kujilinda na kushambulia. Bado anacheza
kuonesha uwezo binafsi kwa kukaa sana na mpira na kuachia wakati tayari
umbo aidha la kulinda au kushambulia limevurugika.
Pia kambi ya Pemba itumike
kutafuta muunganiko mzuri eneo la ulinzi wa kati. Licha ya uimara wa
kiungo cha chini bado Yanga inaonesha kusumbuliwa na jinamizi la kumkosa
mbadala sahihi wa Vincent Bossou. Ni rahisi kuwaamini wakongwe Kelvin
Yondani na Nadir Haroub lakini wanaonesha dhahiri kuianza magharibi ya
soka lao. Usalama wa eneo hilo ni mseto tu . Ni wakati wa kuwandaa vyema
Pato Ngonyani, Shaibu ‘ Ninja ‘ na Andrew Vincent kuwazunguka wakongwe
hao. Nadir kusimama na Dante au Yondani kusimama na Ninja itategemea na
aina ya kiungo wa chini atakayesimama na mfumo wa mwalimu.
Tayari kocha mkuu wa Dodoma FC
iliyopo ligi daraja la kwanza , Jamhuri Kihwelo ‘ Julio ‘ ametanabaisha
ubora wa kikosi cha Yanga kwa kusema wengi wanaipa nafasi ndogo kutetea
ubingwa wake lakini kwake anawaona Yanga bado wa moto.
” kwanza hawajabadili sehemu kubwa
ya kikosi chao hivyo bado wana muendelezo mzuri na pia wamesajili
kulingana na mahitaji hivyo wasiwazuge kuja kinyonge msimu huu hao bado
wa moto ” alisema Julio.
Kauli hiyo ya Julio haipo mbali na
ukweli. Yanga endapo watampata Pappy Tshishimbi kwa wakati na
akaelewana vyema na wenzake hakika watasumbua kwenye ligi. Mathalani
kocha kutengeneza muunganiko wa Pappy kama mlinzi wa chini, juu Kamusoko
au Rafael Daudi , Ajibu 10 na tisa kusimama Ngoma hakika wapinzani
inatakiwa wajipange ukitazama bado Chirwa yupo nje ingawa anaweza pia
kumtumia kama mshambuliaji wa pembeni kwenye 4-3-3 au 3-4-3.
Bado Yanga ni mwendo mdundo kwa msimu wa 2017-18.
Samuel Samuel
Comments
Post a Comment