TaBSA YANDAA MAFUNZO YA BASEBALL KWA WALIMU WA SHULE ZA SEKONDARI DODOMA.

Na Agness Moshi- MAELEZO.
Chama cha Mchezo wa Baseball
Tanzania (TaBSA) kimeandaa mafunzo ya siku mbili yatakayofanyika Agosti
19 na 20 katika viwanja vya Shule za Sekondari mjini Dodoma.
Mafunzo hayo yatatolewa kwa lengo
la kuitikia wito uliotolewa Februari 17, 2016 na Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa uliovitaka vyama vya michezo
Nchini kujiimarisha katika Nyanja mbalimbali ikiwa pamoja na
kuwaendeleza waalimu wazawa kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa.\
Taarifa iliyotolewa Jijini Dar es
Salaam na Katibu mkuu wa TaBSA Bw.Alpherio Nchimbi imeeleza kuwa,
Mafunzo hayo yataendeshwa na mtaalamu wa mchezo huo kutoka Japan kupitia
Shirika la Maendeleo Kimataifa la Japan (JICA) Bw.Hiroki Iwasaki na
yatafunguliwa rasmi Agosti 19 na Mwenyekiti wa Kamati ya michezo ya
Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni katibu tawala wa Mkoa huo.
Mafunzo hayo yatatolewa kwa
nadharia na vitendo kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa timu imara
ya mchezo huo kwa ngazi ya Taifa ambayo itakua ikishikiriki mashindano
ya michezo hiyo ikiwa ni pamoja na mashindano ya Afrika Mashariki mwaka
huu,Dunia kwa mwaka na 2018 na Olimpiki kwa mwaka 2020.
Aidha,Wahitimu wa mafunzo hayo
watakabidhiwa vyeti pamoja na vifaa vya kufundishia mchezo huo ili
wasaidie kukuza uelewa kwa wanafunzi pamoja na wadau wa baseball hapa
nchini.
Katika kuendeleza mchezo huo TaBSA
imefanya juhudi mbalimbali za kukuza na kuendeleza mchezo huo ikiwemo
utoaji wa mafunzo kwa walimu wazawa ambapo hadi sasa wameshatoa mafunzo
katika mikoa ya Mwanza,Kilimanjaro,Mbeya,na Ruvuma.
TaBSA imetoa wito kwa waalimu,
wadau na wapenda michezo kwa ujumla mkoani Dodoma kuhudhuria ili waweze
kuufahamu zaidi mchezo huo, pamoja na kupata ujuzi utakaowawezesha
waalimu kuufundisha kwa ufanisi na weledi zaidi.
Comments
Post a Comment