CHADEMA YAIBUKIA SEIKALI SAKATA LA MAKINIKIA.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu |
Timothy Marko
Chama cha Chadema kimeibuka na kutaja sababu ya ukimya
wa sakata la Makinikia baina ya serikali na kampuni ya Acacia Mining PLC ,
pamoja na kuchelewa kuwasili nchini ndege moja iliyonunuliwa na serikali aina
ya Bombardier, iliyotarajiwa kuingia
mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Wakati akizungumza na wanahabari leo Agosti 18, 2017
jijini Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amedai kuwa
ukimya wa serikali kuhusu sakata la Makinikia, umetokana na Kampuni ya Acacia kufungua
kesi katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi ikidai fidia ya dola za
kimarekani milioni 2, kama hasara iliyopata kutokana na hatua ya serikali
kuzuia makontena yake yenye makinikia kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya
kuuzwa.
“…huko tunakoelekea hali ya nchi yetu itakua mbaya
sana, niseme mengine yanayokuja, sababu ya kubadili sheria tatu na kukatisha
mkataba, kampuni ya Acacia imefungua kesi katika mahakama ya usuluhishi ikidai
dola milioni 2 kama fidia ya hasara iliyoingia wakati mchanga wa dhahabu ulipokamatwa,”
amesema na kuongeza.
“Pia Kampuni ya AngloGold Ashanti, mmliki wa mgodi wa
dhahabu Geita, kwa sababu ya kubadili sheria harakaraka, imetoa taarifa rasmi
ya kutushitaki. Wanakwenda mahakamani ili kudai fidia kwa kila hasara
wanayopata sababu yakubadili mikataba. Nilisema tunaenda kunyolewa mahakamani.
Na taarifa tulizo nazo, makampuni mengine ya uwekezaji katika sekta ya mafuta
na gesi yameanzisha mchakato wa kufungua mashitaka katika mahakama za kimataifa
dhidi ya Tanzania.”
Kuhusu kuchelewa kuwasili ndege, Lissu amedai kwamba
ndege hiyo imezuiliwa kutokana na utekelezaji wa hukumu mbili zilizotolewa na
mahakama ya kimataifa ya usuluhishi, ikiwemo amri ya kukamatwa kwa mali za
Tanzania kufuatia kampuni ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering kushinda kesi iliyofungua mahakamani hapo, ya
kudai fidia ya deni Bilioni 87, baada ya serikali kuvunja mkataba wake wa
ujenzi wa Barabara miaka kadhaa iliyopita.
“ Hadi sasa ndege haijawasili na serikali imepata
kimya cha ghafla. Miaka ya nyuma kampuni ya Stirling ilivunjiwa mkataba wake wa
ujenzi wa barabara na kufungua kesi mahakamani, mahakama iliamuru serikali
ilipe fedha baada ya kushindwa katika kesi. Licha ya jitihada mbalimbali za
kulipwa deni lake, hadi sasa serikali haijalipa,” amesema.
Lissu amedai kuwa,hasara hii siyo mara kwanza kwa nchi
kubebeshwa mzigo wa madeni yanayotokana na maamuzi ya kukurupuka ya mawaziri na
viongozi wa ngazi za juu. Huku akirejea baadhi ya kesi za madai zilizowahi
kufunguliwa dhidi ya serikali, ikiweo ya kampuni ya Sea Tawariq ikitaka fidia
ya bilioni 6 kufuatia meli yake ya samaki kukamatwa na serikali.
Mwanasheria huyo wa Chadema amedai kuwa, kufuatia
hasara hizo, Bunge, vyama vya siasa na wananchi wanatakiwa kuishinikiza
serikali kuweka hadharani kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya nchi, katika
mahakama za kimataifa za usuluhishi ili wananchi wafahamu gharama na hasara
inayoingia taifa.
“Gharama ya serikali kufanya maamuzi ya kukurupuka
bila kuzingatia mikataba na masharti yake iliyosaini na wawekezaji ni kubwa,
kama hivi nilivyozungumzia na anayesema tusiogope kushitakiwa na gharama, huyo
mtu anaitakia nchi balaa na anapaswa kuzomewa na kila mtanzia nayeipenda nchi
yake. Anayefanya maamuzi haya ukishtakiwa unafilisika, hapo ndipo tumefikishwa,”
amesema na kuongeza.
“katiba yetu imetoa majibu, imesema, rais anapofanya makosa ya aina hii
anapaswa kuwajibishwa, katiba imesema rais anapofanya makosa haya anapaswa
kuwajibishwa na bunge kwa kushitakiwa na kuondolewa madarakani, na katiba
imesema rais akiondolewa na bunge na kinga ya mashitaka ya jinai inaondolewa.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema, amedai kuwa “taifa
lolote huongozwa na katiba yake na sheria, tunapopuuza sheria moja kwa moja
tunapuuza mikataba yetu, mtawala wa nchi anapofikiri yuko juu ya mkataba mwisho
wa siku wanaoathirika ni wananchi na si yeye, kauli za kiongozi wa taifa ni za
msingi pale ambapo zinatolewa kulingana na katiba, sheria na mikataba
tunayoingia. Mikata inapokuwa na dosari zipo taratibu za kisheria za kurekebisha
kasoro.”
Comments
Post a Comment