Benki Ya Kilimo Kusaidia Mageuzi Ya Kilimo Njombe

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe.
Christopher Ole Sendeka (katikati) akizungumza na ugeni kutoka Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) walipomtembelea Ofisini kwake Mkoani
Njombe. Ugeni uliongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi
Rehema Twalib (wanne kushoto waliokaa).

Kiongozi wa Msafara wa Ukaguzi wa
Miradi ya Kilimo Mkoani Njombe ambaye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TADB, Bibi Rehema Twalib (Kulia) akiwa na Meneja Ufuatiliaji na
Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe (kushoto)
wakifuatilia kwa makini mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe.
Christopher Ole Sendeka (hayupo pichani).

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe.
Christopher Ole Sendeka akihimiza jambo wakati wa mazungumzo yake na
ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) (hawapo
pichani).

Afisa Mifugo wa Mkoa wa Njombe,
Dkt. George Katemba (watatu kushoto) akizungumza na ugeni kutoka Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania walipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi
ya kilimo mkoani Njombe.

Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania wakiangalia ng’ombe wanaofugwa na Bibi Aloycia Mdenye
mmoja wa wanachama wa cha Wafugaji wa Ngo’mbe wa Maziwa Mkoani Njombe.

Mmoja wa wanachama wa cha Wafugaji
wa Ngo’mbe wa Maziwa Mkoani Njombe, Bibi Aloycia Mdenye (wapili
kushoto) akitoa maelezo kuhusu hali ya ufugaji wa ngo’mbe wa maziwa
mkoani Njombe .
…………………….
Na mwandishi wetu, Njombe
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya
Tanzania (TADB) imesema imejipanga katika kusaidia kuchagiza kusaidia
Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili
kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini kwa wakulima
mkoani Njombe na Tanzania kwa ujumla.
Ahadi imetolewa na Mjumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi ya TADB, Bibi Rehema Twalib wakati alipouongoza ujumbe wa
Benki walipomtembelea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe,
Mhe. Christopher Ole Sendeka mkoani Njombe.
Bibi Twalib alisema kuwa TADB
ilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za kuinua ukuaji wa
uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania ili kuisaidia Serikali
kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya
asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa
kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya
nchi.
Aliongeza kuwa Serikali iliamua
kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia
kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika
sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika kilimo nchini.
“Katika kuhakikisha tunafikia
malengo ya Serikali Benki imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha
inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika
Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa
ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini”
alisema.
Akizungumza na ugeni huo, Mkuu wa
Mkoa huo, Mhe. Christopher Ole Sendeka alisema kuwa ujio wa Benki hiyo
mkoani Njombe kutahamasisha shughuli za kilimo mkoani humo hali
itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa Mhe. Ole Sendeka,
mkoa wa Njombe umejaaliwa rasilimali nyingi kwenye sekta ya kilimo ila
changamoto za ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya
maendeleo ya kilimo zinarudisha nyuma juhudi za wakulima mkoani humo.
“Naishukuru Serikali kwa
kuianzisha TADB kwani hali ya ukosefu wa mitaji ya uhakika inachangiwa
kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa
zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa na kuwasahau wakulima na
wasindikaji wa mazao, hivyo tunaamini TADB itasaidia kutatua changamoto
hii,” alisema.
Bw. Ole Sendeka alitoa wito wa
wakulima mkoani humo kuchangamkia fursa hizo za mikopo ya gharama nafuu
inayotolewa na Benki ya Kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji na hivyo
kujihakikisha kipato cha uhakika.
Kwa upande wake, Meneja
Ufuatiliaji na Tathamini ya Mikopo wa TADB, Bw. Dickson Pangamawe
alisema kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda
Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2
hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi
Miaka Kumi na Mitano (15)).
Kwa mujibu wa Bw. Pangamawe mikopo
hiyo ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia
Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara
ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
“Dhima ya Benki yetu ni
kuhakikisha tunawezesha maendeleo na kufanikisha mapinduzi ya sekta ya
kilimo kwa kutoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwenye miradi ya
kilimo Tanzania inayolenga kukuza uchumi, kuhakikisha usalama wa
chakula na kupunguza umasikini wa kipato,” alisema.
Comments
Post a Comment