HALMASHAURI ZIONGEZE MABWAWA KWA AJILI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI; NAIBU WAZIRI KAMWELWE.

Naibu Waziri
Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa
wa Singida wakisoma kwa umakini taarifa ya Sekta ya maji Mkoa wa
Singida wakati wa kikao na wakuu wa idara mbalimbali.

Naibu Waziri
Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisikiliza
taarifa ya mradi wa maji wa Ughandi kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Singida Edward Kisalu.

Afisa
Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango na Kaimu Afisa
Elimu Mkoa wa Singida Eva Mosha wakimsikiliza Naibu Waziri Wizara ya
Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe.

Kaimu Katibu
Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Baltazar Kichinda akisoma taarifa ya
sekta ya Maji kwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida Buhacha Kichinda.

Naibu Waziri
Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe akisisitiza
jambo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ughandi A
halmashauri ya Wilaya ya Singida alipotembelea eneo la mradi wa maji
kijijini hapo.
………………………………………………………………………………
Naibu Waziri Wizara ya Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isack A. Kamwelwe amezitaka halmashauri za Mkoa wa
Singida kuongeza ujenzi wa mabwawa, utakaosaidia kilimo cha umwagiliaji
ili kuzalisha chakula cha kutosha na kwa ajili ya makao makuu ya nchi,
Dodoma.
Mhandisi Kamwelwe ametoa
maelekezo hayo wakati wa mkutano uliojumuisha wakuu wa idara zote pamoja
na Mkuu wa Mkoa wa Singida ili kujadili hali ya Sekta ya Maji kabla ya
hajaendelea na ziara yake katika halmashauri za Mkoani hapa.
Amesema ardhi ya Singida pamoja
na kiwango cha mvua cha milimita 500 mpaka 800 kwa mwaka vinatosha
kuzalisha chakula kwa ajili ya matumizi ya mkoa lakini ujenzi wa mabwawa
utaongeza uzalishaji wa chakula hasa kwa lengo la kulisha mkoa wa
Dodoma.
“Mkuu wa Mkoa wa Singida una
malengo makubwa na mazuri kwa mkoa huu, mpango wako wa kuifanya Singida
iilishe Dodoma ni mzuri na utafanikiwa hasa mkiongeza bidii katika
uzalishaji na kuweka kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji”, amesema
Mhandisi Kamwelwe.
Ameongeza kuwa Singida inapata
mvua za wastani lakini imekuwa ikizalisha kwa wingi mazao ambayo
yamekuwa yakitumika katika mikoa yote nchini kwa mfano alizeti, viazi
vitamu, vitunguu na asali ambapo mazao hayo yamekuwa yakipendwa kutokana
na ubora wake.
Mhandisi Kamwelwe ameongeza kuwa
hali ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Singida bado inatakiwa
kuboreshwa zaidi kutokana na kuwa kila mwaka serikali imekuwa ikitenga
fedha nyingi lakini asilimia ya upatikanaji wa maji haiongezeki kwa kasi
inayotakiwa.
Aidha amemuomba Mkuu wa Mkoa wa
Singida kusimamia matumizi ya fedha za serikali zinazotengwa kwa ajili
ya miradi ya maji ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa na kwa ubora
mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema kuwa Singida sio kame kwakuwa hakuna
mazao yanayoweza kumea katika ukame isipokuwa Singida imejikita katika
mazao yanayotumia maji kwa ufanisi.
Dkt Nchimbi amesema Singida
inazalisha mazao ya mahindi, alizeti, vitunguu, viazi vitamu na mazao
mengine kwa wingi kutokanana na kuwa mvua zinazonyesha zinatosheleza
kustawisha mazao hayo.
Ameongeza kwa kuwataka wakuu wa
idara zote kusimamia matumizi bora ya fedha za serikali zinazotolewa kwa
ajili ya maji kwakuwa suala la maji ni la kila mmoja na sio kuwategemea
watumishi wa idara hiyo pekee katika kusimamia fedha na miundominu ya
maji.
Dkt Nchimbi amesema Mkoa
unahamasisha uchimbaji wa mabwawa kwa halmashauri, taasisi na hata
makundi mengine kwakuwa mabwawa hayo yatasaidia kuinua kilimo cha
umwagiliaji Mkoani Singida pamoja na kukuza uchumi.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Buhacha Kichinda amesema hali ya upatikanaji wa maji kwa Mjini
ni asilimia 50.6 huku vijijini ikiwa ni asilimia 44 na kuongeza kuwa
wastani huo ni mdogo kwakuwa unarudisha nyuma jitihada za kuinua uchumi.
Kichinda amesema Mkoa umejipanga
kushirikisha wadau zaidi ili kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi ya maji
ya visima virefu pamoja na ujenzi wa mabwawa pamoja na kusimamia fedha
zote za serikali zinazotolewa kwa ajili ya sekta ya maji zinatumika
ipasavyo.
Amesema ili kuhakikisha mvua
zinaendelea kunyesha vizuri pamoja na kutunza vyanzo vya maji, mkoa
umeweka mkakati wa “ Achia shoka Kamata Mzinga” ili kuwahamasisha
wachoma mikaa waache kukata miti bali wajikite katika kutundika mizinga
itakayotunza mazingira.
Comments
Post a Comment